Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

Watafiti wahimiza matumizi ya teknolojia kurutubisha udongo
13 Oct, 2025
Watafiti wahimiza matumizi ya teknolojia kurutubisha udongo

Watafiti wa Udongo wametoa wito kwa wadau wa kilimo hususani wakulima kutumia teknolojia zilizofanyiwa Utafiti zinazolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo ili kusaidia urejeshaji wa rutuba katika udongo na hivyo kuogeza tija katika sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa katika Mkutano wa kimataifa wa mwaka wa 2025 wa Wanachama wa Chama cha wanasanyasi wa Udongo cha Afrika Mashariki (SSSEA) uliofanyika Septemba 29-Octoba 03, 2025 Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Mkutano huo wenye kaulimbiu inayolenga kubadilishana uzoefu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za mifumo himilivu katika nyanda kame wataalamu hao wa udongo walieleza kuwa ikiwa matumizi ya teknolojia zilizofanyiwa utafiti hayatapewa kipaumbele kunaweza kuchangia kuendelea kupungua tija katika kilimo.

Akizungumza katika Mkutano, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Thomas Bwana, alisema suala la afya ya udongo ni muhimu kujadiliwa ikizingatiwa uwepo wa changamoto za mabadiliko ya tabianchi na huku ikifahamika kuwa shughuli za uzalishaji wa chakula zinaanzia katika udongo.

Dkt. Bwana alisema kuwa moja ya mifumo himilivu ni pamoja na kuanzisha kilimo cha mazao mbadala hususani katika maeneo ya nyanda kame ili kuongeza tija hatua ambayo alitaja TARI imeanza utafiti wa zao la Mitende Mkoani Dodoma katika kituo chake cha TARI Hombolo.

Akitaja miongoni mwa sababu zinazochangia changamoto za uharibifu wa rutuba ya udongo Dkt. Bwana alisema matumizi holela ya viuatilu na mbolea bila kufuata ushauri wa kitaalamu inasababisha kuathiri vijidudu rafiki ambavyo hurutubisha udungo.

 

Kukabiliana na changamoto hiyo, Dkt Bwana alisema tangu kuanzishwa kwa TARI,  imegundua teknolojia 343 za kilimo ambapo katika hizo teknolojia nane ni eneo la udongo na maji, teknolojia 15  za uongezaji thamani, teknolojia nane zingine za masuala mtambuka na teknolojia 312 za mbegu bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (ZALIRI) Dkt.  Abdallah Ibrahim Ali alisitiza suala la wakulima kupima afya ya udongo ili kutambua zao linalostahili kulimwa katika maeneo yao badala ya kulima bila kuwa na utambuzi sahihi.

Aidha, Dkt. Abdullah alitoa pongezi kwa serikali ya Tanzania kwa kuwawezesha maafisa ugani vifaa vya kupimia afya ya udongo vilivyopo katika Halmashauri mbalimbali nchini ili kusaidia wakulima kupima afya ya udongo.

Miongoni mwa matukio ya Mkutano huo ni kuchaguliwa  Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Mlingano, Dkt. Mgeta Steven Merumba kuwa mwenyekiti mpya wa chama cha Wanasanyasi wa Udongo cha Afrika Mashariki kwa upande wa Tanzania (SSSEA), akimrithi  Prof. Didas Kimaro, ambaye amekiongoza kwa takribani Miaka kumi.